Watu wasiojulikana wamewaua waandamanaji 11 waliopiga kambi nje ya makao makuu ya Watawala wa Kijeshi Mjini Cairo,Misri.
Maafisa wanasema watu hao walianza kuwashambulia kwa mawe, mabomu na risasi waandamanaji hao ambao pia walijibu mashambulizi hayo. Wanajeshi pamoja na polisi wamezika makabiliano hayo, lakini baada ya saa sita za vurugu.
Abdul Moneim Aboul Fotouh,mgombea wa kujitegemea pamoja na kiongozi wa chama Freedom and Justice Party ambacho kinaungwa mkono na Muslim Brotherhood Mohammed Mursi wamelaani maafisa wa usalama kwa kuchelewa kuzuia fujo hizo.Kufuatia tukio hilo wagombea wawili wakuu wa Urais wamesimamisha kampeini zao kulalamikia mauaji hayo.
Aidha chama cha FJP na kile cha Salafist Nour ambavyo vina wabunge wengi vimesusia mkutano na Baraza tawala la kijeshi{Scaf}.
Maandamano kulalamikia utawala wa kijeshi yameendelea tangu jeshi lichukue madaraka baada ya kuondolewa kwa Rais Hosni Mubarak Februari mwaka 2011.
Watawala wa Kijeshi wamelaumiwa kwa kuwakandamiza wapinzani na kuwaua waandamanaji pamoja na kuzima mashirka ya kiraia.
Watawala wa kijeshi hata hivyo wameahidi kuyakabidhi madaraka kwa raia mwishoni mwa mwezi Juni baada ya kufanyika uchaguzi wa Urais ambao wanasema utakuwa huru na haki.